Saturday, May 12, 2018

SERIKALI YASISITIZA HAKUNA MGONJWA WA EBOLA

Serikali imewatoa hofu Watanzania kuwa hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitika kuwa na virusi vya ugonjwa hatari wa Ebola, lakini Tanzania iko katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo kutokana na mwingiliano wa watu.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). “Nikiri kuwa Wizara imepata taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya DRC kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Lakini hadi sasa hakuna mtu ambaye anahisiwa au kuthibitika kuwa na virusi vya Ebola, kutokana na kupakana na DRC, nataka kukiri kwamba tuko hatarini kuambukizwa ugonjwa huu kutokana na mwingiliano wa watu hawa wanaosafiri kutoka na kuingia Tanzania.” Ummy alisema hatari kwa Tanzania inatokana na kuwepo kwa mwingiliano mkubwa wa wafanyabaishara wanaokwenda DRC, hususani wale wanaotumia njia zisizo rasmi kwa kuvuka Ziwa Tanganyika na mitumbwi. “Napenda kutoa tahadhari kwa wananchi wote.
Tahadhari hii ni kwa nchi nzima lakini hasa katika mikoa ambayo inapakana na DRC, hii iko katika hatari zaidi.” Aliitaja mikoa hiyo ambayo iko katika hatari zaidi kuwa ni Kigoma, Kagera, Mwanza, Katavi, Rukwa na Songwe. Alisema ili kujikinga na ugonjwa wa Ebola, Wizara imeimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko katika mikoa ambayo inapakana na DRC, mipakani na viwanja vya ndege vyote nchini kwa kuweka vifaa vya kubaini joto la mtu (Themo scanner).
Alisema pia wizara imeimarisha mfumo wa ufuatiliaji wagonjwa katika mikoa yote, kusambaza miongozo, vifaa na imeagiza makatibu tawala wa mikoa na wakuu wa mikoa kushiriki katika kutoa taarifa inapotokea dalili zozote. “Niwatake Waganga Wakuu wa mikoa wote lakini hasa hawa ambao wanapakana DRC wasilale, wahakikishe kunakuwa na ufuatiliaji kwa wageni kwa kuweka daftari, mifumo na vifaa maalumu vya kutambua,” alisema. Ummy alisema hivi sasa kuna wodi ambayo imetengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola, watakaobainika katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke.
Alitumia fursa hiyo kuzitaka Hospitali za Rufaa za Mbeya, KCMC mjini Moshi na Bugando jijini Mwanza, kutenga wodi maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa milipuko ikiwamo Ebola. Ummy aliwataka Watanzania kuchukua tahadhari, kwa kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
Pia kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa na Ebola, kuzingatia usafi wa mwili, kuwahi vituo vya afya, kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali katika ngazi zote. Dalili za mgonjwa huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukizwa baada ya siku 2 hadi 21 tangu kupata maambukizi. Dalili hizo ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na vidonda kooni.
Mara nyingi dalili hizi hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi na pia figo na ini kushindwa kufanya kazi. Baadhi ya wagonjwa hutokwa na damu nyingi ndani na nje ya mwili. WHO imetoa taarifa ya kulipuka kwa ugonjwa wa Ebola katika nchi ya DRC katika mji wa Biloko Jimbo la Ikweta, baada ya kubainika kuwapo wagonjwa 21 na 17 kati yao wakiwa wamepoteza maisha. Mwaka jana kulitokea mlipuko wa Ebola katika eneo hilo, ambapo watu wanne walifariki dunia.
Chanzo:HabariLeo 11/05/2018

No comments:

Post a Comment